Mwanamke
mmoja mkazi wa Mchikichini, Mbagala jijini Dar es Salaam, Tatu
Nyambwela (30) anashikiliwa na polisi baada ya kutuhumiwa kumuiba mtoto
mchanga wa miezi mitatu.
Polisi pia inachunguza mtoto wake mwingine wa miaka sita anayeishi naye baada ya kudaiwa kuwa alimpata kwa njia ya udanganyifu.
Taarifa kutoka eneo hilo zinasema mwanamke huyo alikamatwa wiki
iliyopita na kufikishwa katika Kituo cha Polisi Mbagala Maturubai, baada
ya majirani kumtilia shaka.
Akizungumzia tukio hilo, Mwenyekiti wa mtaa huo, Said Pazi, alisema
alipata taarifa hizo kupitia kwa majirani wanaoishi eneo hilo, ambapo
baada ya kujiridhisha aliamua kutoa taarifa polisi.
MTOTO AGUNDULIKA
Akielelezea tukio hilo, alisema walikwenda nyumbani kwa mwanamke huyo
akiwa pamoja na polisi wawili kwa ajili ya kubaini ukweli wa jambo hilo.
Alisema, walipofika katika nyumba anayoishi mwanamke huyo, walimkuta
akiwa amekaa pamoja na mumewe aliyetajwa kwa jina la Adinan Mkanilo
(45), na mama mkwe wake Asha Limbanga (80) wakizungumza.
Mwenyekiti huyo alisema walipomuhoji uhusiano wa mama huyo na mtoto
mchanga, Tatu alionekana kuwa mkali na kueleza mtoto ni wake amemzaa
Septemba 9, mwaka huu.
Alipotakiwa kuthibitisha kauli yake kwa kuonyesha kadi ya kliniki,
hakuweza kuitoa badala yake alisema alimzaa nyumbani, hivyo hakuweza
kupata kadi kama ilivyo kwa watoto wengine.
"Mashaka yetu yalizidi baada ya kuona yule mama hana kadi ya kliniki na
hata tulipomshauri atuletee mtoto tumuone, alikataa jambo ambalo ilibidi
polisi kutumia nguvu kuingia ndani kumuona mtoto," alisema mwenyekiti
huyo.
"Baada ya kufanikiwa kumpata mtoto tulibaini amedanganya umri kwani kwa
mujibu wake mtoto alikuwa wa mwezi mmoja, kitu ambacho siyo kweli,
tulipomuangalia tulibaini alikuwa na umri wa zaidi ya miezi mitatu,"
alisema.
Baada ya kushuhudia hali hiyo, polisi walimkamata mwanamke huyo pamoja
na mume wake na kuwapeleka katika kituo cha Mbagala kwa ajili ya
mahojiano.
Wakiwa kituoni hapo, mama huyo alikiri kwamba mtoto huyo hakumzaa kama
alivyoeleza awali bali alimuiba nyumbani kwao Mkuranga kwa nia ya
kumdanganya mume wake kwamba amejifungua ili kulinda ndoa yake.
MAJIRANI WASIMULIA
Baadhi ya majirani wa eneo hilo walisema waliamua kutoa taarifa hizo
ngazi ya serikali, baada ya kuwa na mashaka juu ya mwanamke huyo, hasa
kutoeleweka vizuri mwenendo wake wakati wa ujauzito na anapojifungua.
Wakizungumza kwa masharti ya kutotajwa majina yao, walisema kwa miaka
mingi, wanamshuhudia mwenzao huyo akiwa anabeba ujauzito na kujifungua
watoto watatu katika hali ya kutatanisha, jambo lilowapa wasiwasi kwamba
hazai kwa njia ya kawaida.
Walisema kila mara wanamuona anakuwa na hali ya ujauzito lakini
inapofikia hatua ya mwisho, anatoweka na anaporejea anarudi akiwa na
mtoto mwenye umri mkubwa.
Walisema jambo lingine lilowatia wasiwasi ni tabia ya mama huyo
kutowanyonyesha watoto wake kama ilivyo kwa akinamama wengine, badala
yake anatumia maziwa ya chupa mpaka mtoto anapokua.
"Unajua hali hii tumeshuhudia kwa mtoto wake wa kwanza, wa pili ambaye
alifariki na huyu wa tatu, ndipo tukaona tujaribu kushirikiana na
viongozi wetu tujue ukweli," alisema mwanamke mmoja.
Alisema safari hii mwanamke huyo kama kawaida yake alipokwenda nyumbani
kwao akiwa mjamzito, alirejea akiwa na mtoto mchanga, lakini
kilichowashangaza wengi ni pale mtoto huyo kuonekana ana umri mkubwa
tofauti na maelezo ya mama yake.
MAMA MKWE: NILIAMINI ANA UJAUZITO
Akizungumzia suala hilo, Asha Limbanga, ambaye mtoto wake ndiye
aliyemuoa tatu, alisema tangu aishi na mkwe wake kwa muda wa miezi sita,
aliamini ujauzito alionao ni halisi.
Alisema, hajaweza kuona kwa uwazi tumbo la mkwe wake, lakini kutokana na
maisha waliyokuwa wakiishi hakuwa na wasiwasi kwamba ipo siku ataletewa
mtoto wa wizi.
Alisema, ilipofikia muda wa kijifunga, aliaga kwamba anakwenda nyumbani
kwao na baada ya kukaa muda wa miezi miwili alirudi akiwa na mtoto huyo
wa kiume.
Hata hivyo, Mkanilo hakupatikana kuzungumzia jambo hilo baada ya
kuelezwa kwamba amekwenda Mkuranga kumpelekea chakula mke wake ambaye
amewekwa mahabusu.
POLISI: TUNAMCHUNGUZA ZAIDI
Akizungumza kwa njia ya simu, Mkuu wa upelelezi Wilaya ya kipolisi ya
Mbagala, aliyejitambulisha kwa jina la Afande Walelo, alikiri kutokea
kwa tukio hilo na kwamba mtuhumiwa amekabidhiwa kwa wenzao wa Mkuranga
kwa ajili ya kumfungulia kesi.
0 comments:
Post a Comment