CHAMA Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimebaini njama ya serikali za kutaka kununua helikopta tatu nchini China kwa ajili ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), huku wakidai kuwa ni mali ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Hayo yamebainishwa jana na Katibu Mkuu wa CHADEMA Dk. Willibrod Slaa wakati akitoa maazimio ya Kamati Kuu ya chama hicho kuhusu mchakato wa Katiba na hatua ya kuipigia kura maoni Katiba inayopendekezwa.
Katika mkutano huo, Dk. Slaa alisema ana taarifa za uhakika kwamba mchakato wa ununuzi wa Chopa hizo tatu, utakamilishwa wakati wa ziara ya Rais Kikwete anayetarajia kuzuru nchi hiyo hivi karibuni.
Katibu Mkuu huyo alisema taarifa alizonazo ni kwamba Chopa hizo zinataka kununuliwa na Rais Kikwete kwa ajili ya kampeni za mgombea urais wa CCM mwakani.
Alisema tayari mkakati unaopangwa na Rais Kikwete umebainika na kwamba hautakubaliwa kwa sababu haujafuata taratibu za sheria za manunuzi nchini.
“Tumebaini mkakati wa wizi wa fedha za walipakodi unaotaka kufanywa na Rais Kikwete …hatutakubali kuona fedha zao zinaliwa na mafisadi huku wakilisingizia jeshi la ulinzi nchini,” alisema Dk. Slaa
Pamoja na hilo, alisema wataendelea kufuatilia na kutoa taarifa kwa umma kwani anayeshughulika na mchakato huo, naye ni fisadi.
Bila kumtaja mhusika wa mchakato huo, Dk. Slaa alisema kilichowashtua hata kufuatilia kwa makini mkakati huo ni mhusika mkuu wa mchakato huo kuwa ni fisadi na unaweza kufanya ufisadi kama ule wa ununuzi wa Rada.
Ziara ya kuikataaa Katiba
Dk. Slaa alisema Chaema inaanza ziara isiyokoma ya kuhamasisha umma wa watanzania kuikataa katiba inayopendekezwa kwani haijatokana na maoni yaliyokusanywa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba.
“Maazimio ya Kamati Kuu iliyokaa siku mbili ni kuunganisha vyama vya siasa, taasisi na umma wa watanzania kushiriki katika kampeni kubwa ili kuhakikisha kampeni ya kuipigia kura ya ‘HAPANA’ katiba inayopendekezwa, inafanikiwa” alisema Dk. Slaa.
Dk. Slaa alisema chama chake kimeamua kufanya ziara ya nchi nzima katika makundi tofauti na kwamba ziara ya kwanza itakuwa ya Baraza la Wanawake wa chama hicho (Bawacha) ambayo itaanza kesho.
Alisema katika ziara hiyo ya siku 20, viongozi wake watahakikisha wanawaelimisha watazania kutambua kuwa Bunge Maalum la Katiba lilitawaliwa na ubabe na usiri uliohakikisha kwamba mchakato wa Katiba unadhibitiwa na serikali na CCM.
“Ziara zetu zitahakikisha zinawaeleza ukweli na madudu yaliyojitokeza ndani ya bunge hilo ikiwamo mchakato wa kutunga sheria za mabadiliko ya katiba ulipindishwa, uteuzi wa wajumbe wa Bunge Maalum kutoka ‘Kundi la 201′ ulifanywa na Rais Kikwete kwa lengo la kuhakikisha wajumbe wengi wanatoka CCM,” alisema.
Dk. Slaa alisema ziara hizo zinawahamasisha watanzania na wapenda mabadiliko kuichagua CHADEMA katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na kuhakikisha wanajiandikisha kwenye Daftari jipya la kudumu la kupigia kura.
Alitumia fursa hiyo kuwakumbusha watanzania kujiandaa kutimiza wajibu wao wa kihistoria wa kukataa uchakachuaji wa maoni ya Katiba, uliofanywa na CCM na washirika wake katika Bunge Maalum la Katiba.
, Dk. Slaa alitoa Rai kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuhakikisha inatekeleza ahadi yake ya kuboresha daftari la wapiga kura kabla ya kufanyika kwa kura ya maoni ya Katiba.
“Tuinataka NEC isimamie kauli yake ili kila mtanzania mwenye haki ya kupiga kura, ajiandikishe kwenye daftari hilo na anapata haki ya kushiriki katika maamuzi ya jambo hilo muhimu kwa taifa,” alisema Dk. Slaa.
CHANZO| Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment