Friday, October 17, 2014

Friday, October 17, 2014

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imewaachia huru watu wawili waliokuwa wakikabiliwa na kosa la kujipatia sh milioni 128.3 kwa njia ya udanganyifu pamoja na kuingilia mawasiliano ya mtandao wa simu.

Hakimu Mkazi, Hellen Riwa, alisema amewaachia huru Aziz Mongi na Edwin Edward baada ya upande wa mashitaka kushindwa kufika na upelelezi kutokamilika.
Kabla ya kuachiwa huru, Hakimu Riwa aliwasomea mashitaka yao ya awali na kudai kuwa kosa la kwanza walilitenda mnamo Agosti 28, 2011 kwenye duka la kubadilishia fedha la Palace Hotel, Ilala jijini Dar es Salaam kwa kufanya njama ikiwa ni kinyume cha kifungu 384(1) cha Sheria ya Kanuni na adhabu sura ya 16 kilichofanyiwa marekebisho 2002.
Alisema kuwa watu hao walitenda kosa la pili kwa kula njama ya kujipatia fedha dola 85,500 za Marekani sawa na sh milioni 128.3 za Kitanzania kutoka kwa mwajiriwa wa duka hilo, Ndenengo Malisa, wakidai wametumwa na mmiliki wa duka hilo Hans Macha.
Hakimu Riwa, alisema shitaka la tatu ni kuingilia mawasiliano ya simu, ambako watuhumiwa hao walitumia namba ya simu ya Macha kwa ajili ya kumdanganya Denengo ili awapatie fedha hizo walizodai wametumwa na mmiliki huyo.
Katika utetezi wake, Mongi alidai kuwa siku ya tukio alifika maeneo ya duka hilo baada ya kumpa lifti mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Beka aliyeingia dukani, huku yeye akiwa hajui kinachoendelea hadi alipokamatwa na polisi.
Kwa upande wa Edward ambaye alikuwa mshitakiwa wa pili, alijitetea kuwa alikuwa yupo likizo akijiandaa na ndoa yake na ndipo alipopigiwa simu na mtu aliyefahamika kwa jina la Beka wakutane kabla ya kukamatwa na polisi.
Baada ya Hakimu Riwa kusoma utetezi wa watuhumiwa hao, alisema Mahakama imeona hawana makosa na kuwaachia huru.

0 comments: