Mkurugenzi Mtendaji wa zamani wa Shirika la Umeme Tanzania (Tenesco), William Mhando
Mahakama imeelezwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa
zamani wa Shirika la Umeme Tanzania (Tenesco), William Mhando, hakuwa
miongoni mwa wajumbe walioshughulikia mchakato wa zabuni iliyopewa
kampuni inayomilikiwa na mkewe kusambaza vifaa vya ofisi katika shirika
hilo.
Shahidi wa upande wa mashitaka, Athanas Kalikamwe, alidai mbele ya
Hakimu Frank Moshi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jana kuwa
wajumbe waliohusika katika mchakato huo ni wale waliotoka katika timu ya
upembuzi na bodi ya tenda.
Alidai kuwa katika taasisi hizi mbili zinazojitegemea, Mhando hakuwa
miongoni mwa wajumbe na kuwa mshitakiwa alihusika katika hatua za mwisho
za utiaji saini wa mkataba huo uliotolewa kwa kampuni ya Santa Clara
Supplies Company Limited.
Kalikamwe alikuwa akihojiwa na upande wa utetezi ukiongozwa na mawakili
Daniel Ngudungi, Alex Mgongolwa, Jamhuri Johnson na Augustine Kusalika
wakati wa kusikiza kesi ya matumizi mabaya ya madaraka inayomkabili
Mhando, mkewe Eva na watumishi wengine wa Tanesco.
Alidai kuwa kama mfanyakazi wa Tanesco, ambayo ni taasisi ya serikali
angepaswa kutangaza maslahi kama angegundua kuwa mmoja wa wazabuni
walioomba angekuwa ndugu yake.
Alidai kuwa waliohusika na mchakato wote kutoka bodi ya tenda na
upembuzi walipaswa kutangaza maslahi kwenye vikao vyao kama wangebaini
kuwa wana uhusiano na kampuni hiyo.
Akiongozwa na Mwendesha Mashikata kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana
na Rushwa (Takukuru), Leonard Swai, shahidi huyo aliwasilisha taarifa ya
upembuzi wa tenda hiyo na nyaraka zingine kama ushahidi kwenye shauri
hilo.
Washitakiwa wengine katika shauri hilo ni France Mchalange na Sophia
Misidai, ambao wote ni wahasibu waandamizi na Naftali Kisinga, ambaye ni
afisa ugavi.
0 comments:
Post a Comment