Thursday, October 2, 2014

Thursday, October 02, 2014

Aliyekuwa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Athuman Livigha.

Mauaji ya Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Athuman Livigha, aliyeuawa kwa kupigwa risasi na watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi nyumbani kwake, Bunju B-Kitunda, Wilaya ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam yamegubikwa na utata.

Utata huo unatokana na maelezo yaliyotolewa na watoto wa marehemu, baba mdogo pamoja na mfanyakazi wake kutofautiana kuhusiana na namna alivyouawa.  Mtoto wa kwanza wa marehemu, Said Athuman, baba yake aliuawa na watu hao usiku wa kuamkia juzi saa 3 usiku wakati anatoka ndani mwake na kwenda kuchukua vinywaji alivyokuwa ameviacha kibarazani.  Said alisema wakati anatoka ndani, watu hao walikuwa nje wakimvizia bila yeye kujua.

Alisema alipofika kwenye kibaraza hicho, watu hao walimpiga risasi moja mgongoni iliyotokea kifuani.Kwa mujibu wa Said, baada ya kupigwa risasi, marehemu alijikongoja na kwenda kufia nje ya nyumba yake.

“Majirani wanaoishi karibu na marehemu walisikia mlio wa risasi saa 3 usiku. Waliogopa kwenda kwenye tukio kutokana kutojua idadi ya wahalifu waliopo pale. Ilipofika asubuhi, nilipata taarifa kutoka kwa mfanyakazi wake,” alisema Said.

Alisema baada ya kufanya mauaji hayo, walitoweka na gari aina ya Toyota Mark II Grand, lenye namba za usajili T 455 CCG, bastola, kompyuta mpakato pamoja na vitu vingine vya ndani.Mtoto wa pili wa marehemu, Selemani Athuman, ambaye anaishi Mwananyamala Kisiwani, jijini Dar es Salaam alisema alipewa taarifa za kifo hicho na ndugu zake siku ya pili.

Alisema taarifa za awali zinasema marehemu alipigwa risasi mgongoni na kumaliziwa na gongo lililokutwa kibarazani.“Baada ya kupigiwa, nilifika eneo la tukio na kukuta polisi wameshafika, ambao maelezo yao ya awali walisema marehemu alipigwa risasi pamoja na gongo mwilini mwake,” alisema Selemani.

Kwa upande wa baba mdogo wa marehemu, Bakari Namanguku, alisema wahalifu walichana nyavu ya dirisha lake ili kumshtua kutoka nje watekeleze kitendo hicho.“Walichana nyavu za dirisha la marehemu wakiwa na nia ya kujua kama marehaemu yupo ndani. Walipongudua hajarudi, walimsubiri na kutekeleza unyama huo,” alisema Namanguku.

Shuhuda wa tukio hilo, Omary Omary, ambaye ni mfanyakazi wa Profesa Livigha alisema alikuta mwili huo juzi saa 3 asubuhi pembezoni mwa nyumba ya marehemu na kuanza kuwapigia simu watoto wake.

Aidha, jirani ya marehemu, Abdulrahman Salum alisimfu Profesa huyo kwa kusema kuwa ni mtu, ambaye alikuwa hapendi utata, dhuluma pamoja na kuishi vizuri na majirani wanaomzunguka.

Marehemu ameacha watoto saba na mwili wake unatarajiwa kuzikwa leo katika makaburi ya Bunju B-Kitunda, saa 7 mchana, jijini Dar es Salaam.

Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova, alipotakiwa na NIPASHE kuzungumzia mauaji ya Profesa Liviga alisema hawezi kuzungumzia tukio hilo na kwamba, anayepaswa kulitolea ufafanuzi ni Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camilius Wambura.

Kamanda Wambura alipotakiwa kulizungumzia tukio hilo alisema anaumwa.Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa huo, Yusuph Mrefu, alisema yuko safarini mkoani Tanga na kuahidi kulizungumzia tukio hilo atakaporudi ofisini.“Mimi niko Tanga. Siwezi kulizungumzia hilo hadi pale nitakaporudi ofisini nitalizungumzia rasmi,” alisema Mrefu.

WAHADHIRI WALIOKWISHAUAWA
 Wimbi la kuuawa kwa wahadhiri vya vyuo vya elimu ya juu nchini limeendelea kuimarika kila siku, huku kizungumkuti cha kesi za ‘majambazi’ wanaosemekana na polisi kuhusika na jinai hizo, zikiwa kwenye mchakato wa maamuzi.

Kumbukumbu za NIPASHE zinaonyesha kuwa katika kipindi cha karibu miaka 10 sasa, wahadhiri wanne wamepoteza maisha katika mikono inayodaiwa na polisi kuwa ya majambazi.

MICHAEL OKEMA
Mwaka 2006, aliyekuwa Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT) , ambaye pia ni Mwandishi Habari Mwandamizi nchini, Michael Okema (52), aliuawa kwa kuchomwa kisu majira ya usiku na kundi lililosadikiwa kuwa la majambazi waliokuwa wamevamia nyumba ya jirani yake maeneo ya Kimara Suka, jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam wa wakati huo, Kamishna Alfred Tibaigana, Okema aliuawa pamoja na jirani yake mwingine walipokuwa katika harakati za kumsaidia jirani yao aliyevamiwa na majambazi.Jirani aliyeuawa pamoja na Okema alikuwa akitiwa Banduka Said.

PROFESA JWAN MWAIKUSA
Julai 13, 2010, Mwanasheria maarufu na aliyekuwa Mhadhiri Mwandamizi wa Shule ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Juani Mwaikusa (58) aliuawa kinyama kwa kupigwa risasi na watu wanaosadikiwa kuwa majambazi.

Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam wakati huo, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Charles Kenyela, alithibitisha kutokea kwa mauaji hayo nyumbani kwa marehemu,  eneo la Salasala, jijini Dar es Salaam.

Kenyela alisema Profesa Mwaikusa alifikwa na mauti baada ya kufika nyumbani kwake akiwa na gari lake aina ya Nadia namba T 876 BEX na kuvamiwa na watu wawili waliosadikiwa kuwa majambazi.

“Wakati Mwaikusa akijiandaa kushuka majira ya saa nne usiku, majambazi hao walimgongea kioo na kumwamru kushuka, lakini Profesa alisita, ndipo majambazi hayo yalipomvuta kwa nguvu na kummiminia risasi,” alisema Kenyela.

DK. SENGONDO MVUNGI
Kama hiyo haitoshi, Novemba 3, 2013 watu waliotuhumiwa kuwa majambazi walimvamia  na kumjeruhi kwa mapanga aliyekuwa Mhadhiri Mwandamizi wa Sheria Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambaye alikuwa pia Mjumbe wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dk. Sengondo Mvungi.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Kova, alisema walifanikiwa kuwatia nguvuni watu sita baada ya siku mbili ya tukio hilo kutokana na msako mkali ulioendeshwa na Jeshi la Polisi.

Hata hivyo, Dk. Mvungi alifariki dunia nchini Afrika ya Kusini, mchana wa Novemba 12, 2013 katika Hospitali ya Millpark Netcare, iliyoko katika jiji la Johannesburg, alikokuwa amepelekwa kwa matibabu zaidi.

0 comments: