Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba,Samuel Sitta.
Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Samuel Sitta
sasa ‘ametangaza rasmi vita’ dhidi ya viongozi wa dini kwa kusisitiza
kuwa hayuko tayari kuwaheshimu wala kuwavumilia ambao wanatoa nyaraka
alizodai kuwa hazina utukufu wa Mwenyezi Mungu kwa waumini wao.
Sitta alitoa kauli hiyo jana asubuhi bungeni wakati akisoma matangazo
mbalimbali na kuamua kusoma waraka aliodai kuwa umetolewa na viongozi
hao wa dini huku akiuhusisha na siasa za kundi la wajumbe waliosusia
Bunge Maalum la Katiba kutoka Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi.
Kundi hilo limejitambulisha kama Umoja wa Kutetea Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Alisema katika mitandao ya kijamii amekuwa akituhumiwa kuwa anawadharau
maaskofu, huku akidai kuwa wakiendelea na matendo kama hayo kamwe
hatawaheshimu.
“Wakiwa na matendo kama hayo, hao maaskofu, itabidi wengine tuendelee
kuwadharau tu, ninao waraka huu ambao umelazimishwa kusomwa ndani ya
makanisa, sioni utukufu wala Ukristo ndani ya waraka huu,” alisema
Sitta.
Alisema kuwa maneno na ujumbe uliomo ndani ya waraka huo unashabihiana
na malengo ya kundi la wajumbe waliounda Ukawa na kususia vikao vya BMK.
Akisoma baadhi ya vipengele vya waraka huo, Sitta alisema kuwa sehemu ya
waraka huo unamlazimisha Rais airudishe Tume ya Mabadiliko ya Katiba na
asitishe mchakato wa Katiba, huku akihoji:
“Tangu lini watu wa kiroho wanatoa maagizo ya mambo ya siasa, hii siyo
haki hata kidogo, lugha iliyoandikwa humu ni lugha ya wale tulio wazoea
ukawa.”
Hata hivyo, baadhi ya wajumbe walilazimika kuomba mwongozo wa
Mwenyekiti, na walipopewa walimshauri Sitta kupatana na viongozi wa dini
kisha awaombe wamuombee kwa Mungu kwa kazi anayoifanya. Mbunge wa
Kishapu, Seleman Nchambi, alisema kuwa anatilia shaka waraka uliosomwa
na Sitta kama kweli ameutoa kwa viongozi wa dini na badala yake akasema
huwa huwenda waraka huo umeokotwa baada ya kuandaliwa na wahuni.
“Sina imani na siamini kama kiongozi wa dini aliyesoma torati, akasoma
Injili, akasoma Quroan na akasoma Biblia, anaweza akayasema maneno hayo
katika nyumba ya Mungu, lakini kama ikitokea na kama imetokea yamesomwa,
basi tusifanane na hao kwa kuwa Mungu anajua tunachokihitaji kabla haya
kumwomba,” alisema Nchambi.
Akitoa mwongozo kwa Nchambi, Sitta alipuuza ushauri aliopewa na badala
yake aliishia kumsifia Mbunge huyo kwa kujitahidi kusoma na kuielewa
Biblia na Quroan.
Kwa upande wake Mjumbe wa BMK kupitia kundi la 201, Oliva Lwena alimuasa
Sitta kutowachukia viongozi wa dini kutokana na yale yanayotokea ndani
ya Bunge akisema kuwa huwenda viongozi hao wanapotoshwa na baadhi ya
vyombo vya habari au baadhi ya wajumbe waliosusia vikao vya bunge hilo.
Badala yake alimtaka baada ya kumalizika kwa shughuli za BMK afanye
ziara ya kutembelea madhehebu mbalimbali ya dini kama alivyofanya wakati
akianza kuongoza Bunge hilo ili kuwaeleza viongozi wa dini hizo mambo
yaliyokuwa yakifanywa na BMK.
“Wakati ukianza kuliongoza Bunge hili ulifanya ziara ya kuwatembelea
viongozi wa dini, hilo lilikuwa jambo jema, inawezekana viongozi hao
hawajui tunachokifanya humu ndani na badala yake wanapata taarifa
kupitia vyombo vya habari au wanapotoshwa na wajumbe waliosusia bunge
hili, nakushauri baada ya shughuli za Bunge hili urudi tena kufanya
ziara ya kuwatembelea ili uwaeleze tulichokuwa tunakifanya humu ndani,”
alisema Lwena.
0 comments:
Post a Comment