HATIMAYE sakata la kuchota fedha kwenye Akaunti Maalum ya Tegeta Escrow, zilizohifadhiwa kwenye Benki Kuu ya Tanzania (BoT), litajadiliwa bungeni Novemba 27 na 28 mwaka huu, imebainika.
Hatua hiyo imefikiwa baada ya Kamati ya Uongozi ya Bunge kukutana juzi, ambapo pamoja na mambo mengine ilijadili na kutengua kitendawili cha kashfa ya mradi wa kuzalisha umeme wa Kampuni ya Independent Power Tanzania Ltd (IPTL), ijadiliwe bungeni.Kikao hicho cha Kamati ya uongozi, kililazimika kujadili sakata hilo kutokana na maagizo ya Naibu Spika, Job Ndugai, aliyoyatoa juzi wakati akitoa mwongozo wa Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kufulila (NCCR-Mageuzi), kutaka Bunge liahirishe shughuli zake ili kujadili sakata la IPTL.Chanzo kutoka ndani ya kikao hicho cha Kamati ya Uongozi, kiliipasha Tanzania Daima kuwa, kamati hiyo imeagiza ripoti zote mbili, kuanzia ile ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kuhusu kashfa hiyo, zijadiliwe bungeni.Uamuzi huo, huenda ukawa mwiba kwa Serikali ambayo juzi kupitia kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, ilisema ripoti ya CAG na Takukuru hazijakamilika, hivyo suala hilo halitajadiliwa kwenye mkutano wa 16 na 17 wa Bunge unaoendelea mjini hapa.Habari zinasema, wenyeviti wa Kamati zote zinazounda Kamati ya Uongozi, walikubaliana na hoja ya Kafulila kutaka ripoti hizo zijadiliwe katika Bunge hili.“Kamati ya uongozi ilianza kikao chake majira ya saa 11 jioni na kumaliza saa tatu usiku. Wenyeviti wa kamati wote, waliungana na hoja ya Kafulila na ikaamuliwa ripoti hizo zijadiliwe Novemba 27 na 28,” alisema mtoa habari wetu.Habari zaidi, zinasema kuwa tarehe ya kujadili ripoti hizo zimewekwa mwishoni ili kuogopa kuharibu ratiba ya Bunge endapo itatokea baadhi ya viongozi kutakiwa kuwajibika.Naibu Spika wa Bunge, Ndugai, alipoulizwa uamuzi wa Kamati ya Uongozi, aliliambia gazeti hili kwamba, kamati hiyo imeamua ripoti hizo zije bungeni katika muda waliopanga.“Ukitaka kujua lini, angalia ratiba ya shughuli za Bunge hili utaiona,” alisema kwa kifupi Ndugai.Wabunge wagawanyikaKutokana na hatua hiyo, wabunge wa Bunge la Jamhuri wamegawanyika katika makundi mawili.Uchunguzi uliofanywa na Tanzania Daima, umebaini kuwa kundi kubwa la wabunge wanahamasishana, tena kupitia vipeperushi kutaka wahusika wa kashfa hiyo wang’oke, huku kundi la pili ambalo ni la wabunge wachache, likipanga mikakati kuwanusuru watuhumiwa.Watuhumiwa katika kashfa hiyo waliotajwa bungeni na Kafulila ni pamoja na Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo, Katibu Mkuu wake, Eliachim Maswi, Waziri wa Fedha Saada Mkuya, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Prof. Benno Ndulu, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umeme nchini (Tanesco), Mhandisi Felchesmi Mramba.Sakata hilo liliibuka tena juzi siku ya kwanza bungeni, baada ya Kafulila kuomba mwongozo wa Spika kutaka Bunge liahirishe shughuli zake ili kupata fursa ya kujadili ripoti ya CAG na Takukuru za uchunguzi wa kashfa hiyo.Kabla ya Naibu Spika Ndugai kutoa mwongozo wake, Waziri Lukuvi alipinga mwongozo huo kwa madai kuwa ripoti hizo hazijakamilika.Kauli ya Lukuvi, ilimuibua Mbunge wa Muhambwe, Felix Mkosamali (NCCR-Mageuzi), ambaye aliibana Serikali ilete ripoti hizo bungeni, vinginevyo Dodoma hapatakalika.Mbunge wa Kigoma Mjini, Peter Serukamba (CCM), akichangia hoja hiyo, alilitaka Bunge kuunda Kamati Teule kuchunguza kashfa hiyo wakati Serikali kupitia kwa CAG na Takukuru ikiendelea na uchunguzi wake.Akitoa mwongozo wake, Naibu Spika Ndugai, alisema kwa kuwa Kamati ya Uongozi ya Bunge ilitarajiwa kukutana juzi jioni, ambapo pamoja na mambo mengine itajadili hoja hiyo ya IPTL na kutolea ufumbuzi.Tayari nchi wahisani zimetangaza kuikatia misaada Serikali ya zaidi ya sh trilioni 1 kutokana na kashfa hiyo.Akaunti ya Tegeta Escrow ilifunguliwa kutokana na kutoelewana kuhusu gharama halisi na halali za umeme unaozalishwa na IPTL na kuuzwa kwa Tanesco.Mahakama ya Usuluhishi ya Kimataifa (ICSID), katika uamuzi wake wa Februari 2014, ilitoa hukumu kuonyesha kwamba Tanesco walitozwa kiwango cha juu zaidi ya kilichopaswa kulipwa kwa IPTL.Kwa uamuzi huo, ni dhahiri kwamba fedha zilizokuwa zimehifadiwa kwenye akaunti hiyo maalumu ya Escrow zilipaswa kugawanywa kwa IPTL na Tanesco baada ya hesabu kufanyiwa marekebisho upya kwa viwango halali, lakini badala yake fedha hizo zilitoweka ghafla kwenye akaunti hiyo.
CHANZO: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment