Wednesday, April 1, 2015

Wednesday, April 01, 2015

Mkuu wa Mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo (pichani) amewataka watumishi wa  umma pamoja na watendaji wa Halmashauri  kuachana na tabia ya kuwa na itikadi ya vyama vya siasa ambayo wakati mwingine inaleta migogoro na badala yake wajikite zaidi katika kuwatumikia wananchi wao pamoja na kushiriki kikamilifu katika shughuli za kuleta maendeleo na sio vinginevyo.



Injinia Ndikilo ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na watumishi  wa umma pamoja na madiwani wakati alipofanya ziara ya kikazi ya siku moja  katika Wilaya ya Mkuranga  yenye lengo la kubaini cangamoto zinazowakabili pamoja na kukagua miradi mbali mbali ya maendeleo mkoani humo.
Amesema kwamba watumishi wa umma wamekuwa wakilipwa mshahara kutokana na kufanya kazi, hivyo wanapaswa kuwatumikia wananchi wao kwa nguvu zote na sio kutumia muda mwingi katika kubishana katika mambo hayana msingi wowote na tija kwa maendeleo ya mkoa na taifa kwa ujumla.
Aidha Ndikilo ametoa muda wa siku tatu kwa wazazi na walezi wenye watoto ambao wamefaulu kuingia kidato cha kwanza lakini  hadi sasa bado wapo majumbani kwao kuwapeleka haraka iwezekanavyo, na kama wakishindwa basi atawachukulia hatua kali za kisheria kwa kuwakamata na kuwapeleka katika vyombo vya dola.
Kwa upande mwingine, Makamu Menyekiti wa Halmashauri  ya Mkuranga Juma Abeid,ambaye hakusita kumweleza Mkuu wa Mkoa wa Pwani kilio chao,pamoja na  changamoto ambazo zinawakwamisha katika kutekeleza kwa wakati miradi  mbali mbali ya maendeleo.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga Abdalah Kiato awali akisoma ripoti ya utekelezaji kwa Mkuu wa Mkoa naye alikuwa na haya ya kusema,; "Wilaya ya Mkuranga ambayo kwa sasa ina idadi ya watu zaidi ya laki mbili bado inakabiliwa na changamoto mbali mbali ikiwemo kutokamilisha ujenzi wa maabara katika shule za sekondari, wazazi kutowapeleka watoto  wao shule, miundombinu ya barabara kuwa mibovu pamoja na hali ya kuwepo kwa wimbi la kuwepo kwa bandari bubu ambazo zimekuwa ni kikwazo cha muda mrefu".

0 comments: