Wednesday, April 1, 2015

Wednesday, April 01, 2015
                               
                                      Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Henry Mwaibambe

Jeshi la Polisi Mkoa wa Kagera linawashikilia watu wawili kwa tuhuma za kukutwa na viungo vya mtu mwenye ulemavu wa ngozi (albino). 

Watu hao wanatuhumiwa kufukua kaburi la mtu huyo na kuchukua kila kiungo cha mwili wa mtu huyo aliyejulikana kwa jina la Bartazar John, aliyefariki mwaka 1991.
Hatua hiyo imechukuliwa na jeshi hilo zikiwa zimepita siku saba tangu watu wengine wawili kutiwa nguvuni kwa tuhuma za kuhusika  kuuza viungo vya marehemu Wilaya ya Muleba, mkoani humo.
Kamanda wa Polisi mkoani humo, Henry Mwaibambe, alisema watu hao walikamatwa Machi 27, mwaka huu, katika nyumba moja ya kulala wageni, iliyoko eneo la Kyaka, Wilaya ya Missenyi baada ya kukutwa wakiwa na baadhi ya viungo hivyo, ambavyo walikuwa wanakwenda kuviuza.
Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Laston Faustine (41), ambaye ni mkazi wa Lukulaijo aliyekutwa na mfuko uliokuwa umehifadhi mifupa mitatu ya binadamu na mwingine ni January Korongo (43), mkazi wa Kadengesho, wiyani Karagwe.
Kamanda Mwaibambe alisema baada ya kumbana, mtuhumiwa wa kwanza, Laston aliliambia Jeshi la Polisi kuwa aliyempa viungo hivyo ni mwenzake, January, kwa ajili ya kuviuza kwa Sh. milioni 20.
Baada ya kuhojiwa, January alikiri kufukua kaburi la mjomba wake, aitwaye Baltazari aliyekuwa na ulemavu wa ngozi albino pia mlemavu wa viungo, ambaye alifariki dunia mwaka 1991 na walifukua kaburi lake mwaka 2009.
Mwaibambe alisema baada ya kumhoji zaidi mtuhumiwa huyo, alikubali kuongozana na polisi hadi nyumbani kwake, ambako alionyesha fuvu la kichwa, mifupa mitatu ya miguu pamoja na mifupa ya sehemu mbalimbali, ambayo ilikuwa imefungwa kwenye mfuko nje ya nyumba yake.
Polisi waliomba kibali cha Mahakama Wilaya ya Karagwe kuruhusiwa kufukua kaburi hilo ili kuhakikisha kama kweli kuna mabaki ya mwili huo, lakini hakuna kilichopatikana.

0 comments: