TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imeweka historia na kujenga heshima ya taifa kwa kuweza kuandikisha wananchi katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa Mfumo wa BVR kwa mafanikio makubwa na kuyashangaza mataifa makubwa duniani.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kufuatilia Masuala ya Uchaguzi Tanzania (TEMCO), ambaye pia ni Mkuu wa Ujumbe wa Kufuatilia Masuala ya Uchaguzi, Dk Benson Banna,(pichani) alisema Dar es Salaam jana kuwa NEC inastahili pongezi kubwa kwa hatua hiyo.
Katika kufanikisha hilo, Chama Cha Mapinduzi (CCM), Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Chama cha Wananchi (CUF) vimetajwa kuwashawishi wanachama na wafuasi wake kwa kiwango kikubwa kujiandikisha katika BVR.
Alisema utafiti uliofanywa na Temco kwa kupitia vituo 8,398 vya uandikishaji ambavyo ni asilimia 80.5 ya vituo vyote, umedhihirisha kuwa kazi hiyo ilifanyika kwa ukamilifu kwa wananchi wengi kupata nafasi ya kujiandikisha huku asilimia 64 ya vituo vikizidisha hadi muda wa kufunga katika kuwawezesha wananchi kujiandikisha.
Kwa hatua hiyo, Dk Banna alisema NEC imefuta aibu kwa Taifa, kutokana na mataifa mbalimbali ya nje kubeza uwezo wa nchi katika kufanikisha uandikishaji huo kabla ya kuanza na kwamba sasa kama Taifa, Tanzania imeanza kuonesha uwezo mkubwa wa kujitegemea katika uendeshaji wa shughuli za uchaguzi.
"Hili lazima nilisema wazi, ni aibu kwa mataifa makubwa kufadhili shughuli za uchaguzi maana kitendo hicho ni hatari kwa nchi kuweza kujiamulia mambo yake na kukuza demokrasia ya kweli, hivyo NEC wanastahili pongezi," alisema Dk Banna.
Akielezea mlolongo mzima wa uandikishaji, mwanazuoni huyo alisema, Temco katika ufuatiliaji wake huo ilibaini kasoro mbalimbali ikiwemo fedha kutolewa kidogo na kwa kuchelewa hatua iliyofanya tarehe ya kuanza kwa uandikishaji kuchelewa na kusababisha usumbufu kwa wananchi.
Alisema pia wakati tathimini ya awali ilikuwa ni kuhitajika kwa visanduku vya BVR zaidi ya 15, 000, serikali ilikataa pendekezo hilo na kusema visanduku vinavyohitajika ni 14,000, lakini hata hivyo havikuweza kununuliwa badala yake vilinunuliwa visanduku 8,000 tofauti na ushauri wa NEC ambayo ilishauli kiwango cha chini kiwe visanduku 10,000.
0 comments:
Post a Comment