Serikali ya Tanzania na Poland zimeingia makubaliano ya ushirikiano yatakayosaidia kukuza sekta ya kilimo kwa kuwawezesha wakulima kupata zana bora za kilimo kupitia Kampuni ya kutengeneza Matrekta ya Ursus kutoka nchini Poland itakayoanza kufanya kazi zake nchini Tanzania mwanzoni mwa mwaka 2016.
Akizungumza mara baada ya kufanyika kwa mkutano wa makubaliano hayo kati ya Serikali ya Tanzania na ujumbe wa wataalam wa kilimo kutoka nchini Poland ulioongozwa na Waziri wa Kilimo na Maendeleo Vjijini wa Poland Bi. Zofia Szalczyk jana jijini Dar es salaam, Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika, Stephen Wasira (pichani juu kulia) alisema kuwa makubaliano hayo yanalenga kuinua sekta ya kilimo na kurahisisha upatikanaji wa matrekta hapa nchini.
Alisema Kampuni ya kutengeneza Matrekta ya Ursus kutoka Poland imepewa jukumu la kuleta vipuri vya matrekta na kuviunganisha hapa hapa nchini ikishirikiana na Shirika la Uchumi na Maendeleo la Jeshi la Kujenga Taifa (SUMA JKT).
“Tumeingia mkataba na Seikali ya Poland ili kuinua na kuimarisha sekta ya kilimo nchini kupitia uundwaji wa matrekta haya hapa nchini, kazi hii itasaidia kupunguza kilimo cha jembe la mkono ambacho kinafikia asilimia 62 na asilimia 38 iliyobaki inajumuisha kilimo cha jembe la kukokotwa na wanyamakazi “plau” pamoja na matrekta” Alisema.
Aliongeza kuwa Serikali itawajengea uwezo SUMA JKT ili waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo na kuondoa hali iliyopo ya uagizaji wa matrekta yaliyounganishwa ambayo hutumia gharama kubwa na kusababisha wakulima wengi hushindwa kumudu gharama ya kuyanunua.
“Wakulima wataunganishwa na Benki ya kilimo nchini kwa kupewa mikopo mbalimbali ya kununua vifaa vya kutendea kazi mbegu pamoja na mbolea ili kukifanya kilimo kiwe cha kisasa zaidi” alisema Wasira.
Wasira alisema kuwa Maghala yaliyopo nchini yanauwezo wa kuhifadhi chakula tani 240,000 baada ya kukamilika ujenzi wa maghala hayo kutakuwa na uwezo wa kuhifadhi tani 446,000 za chakula ambapo zitatumika Dola za Kimarekani milioni 110 katika ujenzi wa maghala hayo.
Aidha, Wasira aliongeza kuwa ili kuwa na mafanikio katika sekta ya kilimo nchini, Serikali itapeleka wataalamu wa matrekta kila mkoa.
Kwa upande wake Waziri wa Kilimo na Maendeleo Vjijini wa Poland Bi Zofia Szalczyk alisema kuwa hatua iliyofikiwa na Serikali ya Tanzania ni ya muhimu katika katika kuongeza tija katika uzalishaji kupitia sekta ya kilimo.
Alisema Poland imefanikiwa katika sekta ya kilimo kwa sababu inashirikiana na taasisi za kifedha za kimataifa ambapo ameisifu Tanzania kuchukua uamuzi huo ambao utaiwezesha kuwa na kilimo chenye tija.
Adha, ameishukuru Serikali ya Tanzania kupitia Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika pamoja na Waziri wa Fedha nchini na kuahidi kuendelea kuimarisha uhusiano kati ya nchi hizo mbili katika masuala mbalimbali ya kijamii, kiuchumi na kisiasa.
0 comments:
Post a Comment