Mgombea urais kwa tiketi ya CCM, John Magufuli (pichani kulia), amesema ana uhakika wa kuingia Ikulu kwenye uchaguzi wa Oktoba 25, mwaka huu na kwamba hata wapinzani wake katika kinyang'anyiro hicho wanajua hilo.
"Ikulu ni ya Magufuli. Ninasubiri tu kuapishwa...hata wapinzani wangu wanajua kwamba wao wameshashindwa na vyombo vya habari siku ya kuapishwa viripoti hivyo kwamba mimi ndiye mshindi."
Dkt. Magufuli alitoa kauli hiyo katika mkutano wa kampeni uliofanyika katika Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma,mkoani Dodoma jana.
"Naenda Ikulu nikapambane na mafisadi wanaozuia hela zikae juu zisiwafikie Watanzania," alisema Dkt. Magufuli na kusisitiza kwamba anachukia rushwa na ufisadi kwani ndivyo vinavyokwamisha maendeleo ya Watanzania.
Alisema akiingia Ikulu atahakikisha anajenga kiwanda kikubwa kila mkoa ili kutengeneza ajira kwa vijana na kutokana na tabia ya kuuza bidhaa ghafi.
"Hili nitalisimamia kwa nguvu zangu zote na akili zangu na nitawapa fursa wawekezaji waweke pesa za kutosha nchini ili kutengeneza fursa za ajira na kuwapa watu maendeleo.
Kuhusu ardhi, alisema akiwa madarakani itakuwa marufuku mtu kuchukua ardhi ya mtu bila kumlipa fidia, kwani kufanya hivyo ni kukwamisha maendeleo ya Watanzania wa hali ya chini.
Alisema yeye anaheshimu sheria na anapenda kusimamia sheria ili kuhakikisha Watanzania wanatendewa haki.
Aliongeza kuwa CDA wanachukua mashamba au viwanja vya watu hawalipwi fidia zao wanazostahili; hivyo katika Serikali yake ni marufuku kuchukua ardhi ya mtu bila kulipa fedha anayotaka.
"Tatizo kubwa ni kwamba halmashauri na mamlaka hiyo wote wanataka kipima viwanja; na kusababisha mgongano wa kimasilahi miongoni mwao," alisema Dkt. Magufuli. Alisema Serikali yake itakuwa ya viwanja na kupunguza vifaa vya ujenzi.
Kwa upande wake Waziri Mkuu Mstaafu, Jaji Joseph Sinde Warioba, amesema tatizo kubwa la nchi hii ni ufisadi; hivyo mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. John Magufuli, ana uwezo mkubwa wa kusimamia na kuongoza taifa kutokana na uadilifu wake.
Pia alisema Dkt, Magufuli ana uwezo mkubwa wa kuunganisha Watanzania na kwamba kitendo chake cha kuhubiri na kudumisha amani ni wazi kuwa ni mzalendo wa kweli katika nchi hii.
"Ndugu zangu wananchi, kama wengine hawajui, Tanzania ndiyo nchi pekee ambayo imefanikiwa kulinda amani na utulivu ndani ya miaka 54 ya uhuru wa nchi yetu, hivyo ni muhimu sana kuendelea kuhubiri amani katika nchi," alisema Jaji Warioba.
Aliwataka vijana kulinda amani na kuongeza kuwa waliopambana kuleta amani iliyopo ni vijana, huku akimtaja Mwalimu Julius Nyerere wakati akidai uhuru wa nchi.
Alisema kuwa kama kuna kiongozi yeyote hajui historia ya nchi hii basi huyo hafai kuwaongoza Watanzania, huku akidai zamani kutoka Dar es Salaam hadi Mbeya ilikuwa shughuli kufika, lakini leo baadhi ya wanasisa wanadai katika kipindi cha miaka 54 hakuna kilichofanyika.
Naye Makamu Mwenyekiti mstaafu na waziri mkuu mstaafu wa awamu ya pili John Malecela aliwataka Watanzania kumpigia kura Dkt. Magufuli kama kweli wanahitaji aende Ikulu. Alisema kuwa hawezi kwenda Ikulu kama hawajashikamana na kuhimizana kwenda kupiga kura itakapofika Oktoba 25, mwaka huu.
0 comments:
Post a Comment