Wednesday, October 8, 2014

Wednesday, October 08, 2014

Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake  la Chadema (Bawacha) na Mbunge wa kawe,Halima Mdee (mwenye suti nyeusi) na wafuasi wengine wa Chadema  wakisindikizwa kupanda gari la polisi baada ya kutokamilika kwa dhamana yao katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es salaam jana. 

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha) na Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (35), jana alikosa dhamana na kupelekwa rumande katika Gereza la Segerea hadi leo maombi ya dhamana yake yatakaposikilizwa tena.
Mdee pamoja na wenzake wanane, walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka mawili likiwamo la kutotii amri halali ya Jeshi la Polisi na kufanya mkusanyiko usio halali.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi, Janeth Kaluyenda washtakiwa hao waliyakana yote na upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika, hivyo kuiomba Mahakama kupanga tarehe ya kuwasomea washtakiwa maelezo ya awali.
Hakimu Kaluyenda alisema dhamana ipo wazi na kila mmoja asaini bondi ya Sh1 milioni na kuleta wadhamini wawili ambao mmoja kati yao awe anafanya kazi katika taasisi inayotambulika kisheria.
Pia alisema wadhamini hao wawasilishe barua kutoka kwa waajiri wao na kitambulisho cha kazi. Hata hivyo, upande wa mashtaka uliiomba Mahakama kuwapa nafasi ya kwenda kukagua nyaraka za dhamana zilizowasilishwa na wadhamini wa washtakiwa hao, ombi ambalo lilikubaliwa.
Baada ya kutoa masharti hayo Hakimu Kaluyenda aliahirisha kesi hadi Oktoba 21, mwaka huu kwa ajili ya washtakiwa hao kusomewa maelezo ya awali, kisha hakimu huyo aliondoka kabla ya mchakato huo wa uhakiki kumalizika.
Mawakili wa Serikali waliporudi jioni, iliwalazimu mawakili wa washtakiwa, Mabere Marando na Peter Kibatala kutoa ombi kwa Hakimu Mfawidhi, Isaya Halfani kuwa washtakiwa hao waachiwe na kwenda kulala nyumbani ili leo wafike mahakamani lakini mawakili wa Serikali walipinga ombi hilo.
Kutokana na pingamizi hilo, Hakimu Halfani aliahirisha kesi hiyo hadi leo saa 3:00 asubuhi kwa ajili ya dhamana na kuamuru Mdee na wenzake kupelekwa rumande.
Akisoma hati ya mashtaka, Wakili wa Serikali, Bernard Kongola aliwataja washtakiwa wengine kuwa ni Rose Moshi (45), Renina Peter ‘Lufyagila’, Anna Linjewile (48), Mwanne Kassim (32), Sophia Angel (28), Edward Julius (25), Martha Mtiko (27) na Beatu Mmari (35).
Kongola alidai kuwa washtakiwa hao Oktoba 4, 2014, wakiwa Mtaa wa Ufipa, walikiuka amri halali ya kutawanyika iliyotolewa na Mrakibu wa Polisi (SP), Emmanuel Tillf kwa niaba ya Jeshi la Polisi.
Alidai kuwa, washtakiwa hao walifanya kosa hilo kinyume na Kifungu cha 124 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Katika shtaka la pili, siku hiyo ya tukio katika eneo hilo, washtakiwa hao wanadaiwa kuwa kwa pamoja, walifanya mkusanyiko usio halali kwa lengo la kutembea kwenda kwenye Ofisi ya Rais. Alidai kuwa kosa hilo ni kinyume na Kifungu cha 74 na 75 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

CHANZO: MWANANCHI

0 comments: