TAARIFA RASMI
Katika
gazeti la Jamhuri la Jumanne Agosti 19 – 25, 2014 ISSN No. 1821-8156
Toleo No. 150, zilichapishwa taarifa potofu zenye kichwa cha habari;
KASHFA IKULU;
· Nyalandu atumia Leseni ya Rais kuua wanyamapori 704 bure,
· Watakaouawa wamo pia tembo 8, chui 8, Simba 8, ndege,
· Wauaji ni Wamarekani marafiki wa Waziri wa Maliasili.
I.
Wizara ya Maliasili na Utalii inapenda kuwafahamisha Umma kuwa, tuhuma
hizi si za kweli. Tuhuma hizi zimetolewa na watu wenye nia ovu na
zimelenga kuchafua jina la Wizara ya Maliasili na Utalii na kumchafua
mheshimiwa Waziri Lazaro Nyalandu, kumshushia Heshima, kumdhalilisha kwa
umma ili kumpunguzia dhamira, malengo na kasi ya kupambana na
ujangili.
Ukweli ni kwamba Familia ya
Freidkin ilipewa Leseni Maalum/Leseni ya Rais (Special
License/President’s License) ya kuwinda kwa mujibu wa Kifungu cha 58 (1)
cha Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori Na. 5 ya mwaka 2009 ikisomwa kwa
pamoja na Tangazo la Serikali Na. 273 la mwaka 1974 ambacho kinampa
mamlaka Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori baada kupata ridhaa ya Waziri
mwenye dhamana ya Wanyamapori kutoa kibali maalum kwa malipo au bure.
Aidha, kibali hicho hutolewa baada ya Waziri kuridhika kwamba kibali
hicho kina maslahi kwa taifa na hakikinzani na sheria na mikataba ya
kimataifa kama CITES.
Kufuatana na Kifungu hicho cha 58 (1) Leseni Maalum hutolewa kwa mtu yeyote kwa masilahi ya kitaifa ikiwemo:-
1. Utafiti wa kisayansi
2. Makumbusho
3. Elimu
4. Utamaduni na
5. Chakula wakati wa dharura
Maslahi ya taifa ni pamoja na
leseni kutolewa kwa watu mashuhuri kama vile Wakuu wa nchi, Wafalme,
Malkia, Wakuu wa dini pamoja na watu ambao katika utendaji wao wametoa
michango yenye manufaa maalum kitaifa au michango mikubwa katika
shughuli za uhifadhi wa wanyamapori.
Katika utaratibu huu, kwa mwaka 2013 hadi sasa, Leseni ya Rais zimetolwa kwa watu wafuatao:-
Na. Jina Kibali Na. Kampuni iliyowindisha Bure/Malipo
1 H.H. Sheikh Abdullah Mohamed Buli Al Hamed 000000657 cha
22/8-6/09/2013 Kilombero North Safaris/Green Mile Safaris Bure
2 H. H Sheikh Mohamed Rashid Al Maktoum 0000676 cha 16/01 –
26/01/2014 Ortello Business Corporation (OBC) Bure
3 Familia ya Freidkin ya Watu wanane 00006678-85 za
1-21/08/2014 Tanzania Game Trackers Safaris Ltd Kwa malipo
4 Kiongozi wa Bohora Duniani Bure
Familia ya Freidkin imekuwa na
sifa ya kupewa Leseni ya Rais kutokana na mchango wake mkubwa kwa taifa
katika shughuli za uhifadhi wa Wanyamapori kwa kipindi cha zaidi ya
miaka ishirini iliyopita bila kukoma.
Familia ya Freidkin imekuwa ikitoa
mchango huo kupitia Kampuni ya Uwindaji wa Kitalii iitwayo Tanzania
Game Trackers Safaris Ltd. Pamoja na Asasi yake iitwayo Freidkin
Conservation Fund (FCF tangu miaka ya 1990).
FCF imekuwa ikitoa michango mikubwa hususan ya kukabiliana na ujangili.
Bw. Freidkin kwa kupitia Taasisi hii amekuwa akichangia na hata
kushiriki katika shughuli za kuzuia ujangili na shughuli za kijamii kwa
kufanya yafuatayo:-
a. Kwa kushirikiana na
watumishi wa Idara ya Wanyamapori katika kazi za kuzuia ujangili amekuwa
akichangia mafuta ya doria katika Mapori ya Akiba ya Kizigo, Maswa,
Moyowosi, Ugalla na Pori Tengefu la Lake Natron
b. Kutoa magari ambayo hutumika kwenye kuzuia ujangili
c. Kutoa helikopta kwa ajili ya kufanya doria kwenye mapori husika
d. Kuchangia malipo ya doria kwa askari wa Idara.
e. Kuchangia katika shughuli za maendeleo ya jamii kama vile
kujenga vituo vya doria (outposts) na ujenzi wa shule mpya (kwa mfano
Kizigo Sekondari/Manyoni)
Vibali vilivyotajwa na Gazeti la
Jamhuri la tarehe 19/08/2014, Toleo la 150 vilitolewa kwa familia ya
Freidkin ya watu wanane (8) kwa ajili ya uwindaji kuanzia tarehe 1 hadi
21 Agosti 2014 kwenye vitalu vya Lake Natron, Makao open na Makao
Wildlife Management Area (WMA), Maswa Kimali na Maswa Mbono kupitia
kampuni ya Tanzania Game Trackers Safaris Ltd
Maeneo hayo yaliyowindwa
hayahusiani na ugawaji wa vitalu kama ilivyoelezwa na gazeti la Jamhuri
ya kuwa Waziri Nyalandu amegawa vitalu zaidi ya vitano kwa kampuni
moja.. Leseni ya Rais inatuma kuwinda katika sehemu yoyote ile
itakayoonekana inafaa kisheria bila kujali idadi ya vitalu husika kwa
vile ni shughuli ya mara moja tu.
Uchambuzi wa makala ya gazeti hili ulitaja vipengele kama:-
a) Gazeti la Jamhuri liliandika taarifa potofu yenye kicha cha habari; KASHFA IKULU
Gazeti la Jamhuri liliandika taarifa potofu kuwa, Waziri wa
Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu ametumia Leseni ya Rais kuwaruhusu
marafiki zake Wamarekani wanane kuua wanyamapori 704 bila kulipa hata
shilingi moja serikalini.
Tuhuma hizi si za kweli.
Ukweli ni kuwa, Pamoja na leseni hii kuitwa Leseni ya Rais kwa
Mujibu wa Tangazo la Serikali Na. 273 la mwaka 1974, leseni hiyo
haitolewi na Ikulu bali hutolewa na Mkurugenzi wa Wanyamapori baada ya
kupata ridhaa ya Waziri mwenye dhamana ya kusimamia Maliasili na Utalii
na leseni hiyo haikutolewa bure.
b) Tuhuma zilizotolewa na
gazeti la Jamhuri dhidi ya Waziri Nyalandu ya kuwa ametoa leseni ya Rais
kwa rafiki zake Freidkin na familia yake pia si za kweli.
Leseni ya Rais ilitolewa kwa
familia ya Freidkin na Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori kwa kuzingatia
utaratibu kama walivyopewa watu wengine ambao wamekidhi vigezo kama
ilivyoelezwa hapo juu.
Tuhuma zilizotolewa na gazeti la
Jamhuri dhidi ya Waziri Nyalandu ya kuwa ametoa leseni la kuwinda
wanyamapori 704 bila malipo pia si za kweli.
Ukweli ni kuwa, si kweli kwamba
familia ya Freidkin ilipewa leseni bila malipo kwani familia hiyo
ilipewa Leseni ya Rais baada ya kulipia ada ya vibali (permit fee), ada
ya nyara (trophy handling fee) na ada ya uhifadhi (conservation fee) na
ada ya wanyamapori watakaowindwa ambayo ingelipwa baada ya uwindaji
kufanyika kama ilivyo kwenye Kanuni za Uwindaji wa Kitalii (GN No. 243
Kanuni 21 (1),
Utaratibu huu unatumika kwa wawindaji wote wa kitalii.
Idadi ya wanyamapori wanaotolewa
kwenye leseni yoyote kupitia kampuni za uwindaji wa kitalii hutolewa kwa
kufuata “Safari Package” na siyo wote wanaowindwa kwa kuwa uwindaji ni
wa kuchagua kwa kuzingatia ukubwa na ubora wa nyara, umri, jinsia na
iwapo wamepatikana eneo husika. Hivyo kama mwindaji anashindwa kupata
mnyama mwenye sifa hizo ni kwamba hatawinda mnyama husika hata kama
ameandikwa kwenye leseni. Hii ndiyo tasfiri ya kisheria ya kulipia
wanyama watakaowindwa tu na siyo wanaoandikwa kwenye leseni/kibali.
Aidha, kulingana na sheria,
mwindaji anatakiwa kuandika kila mnyama anayewindwa nyuma ya leseni mara
tu baada ya kuwinda kwa kuonesha tarehe mnyama alipowindwa, aina ya
mnyama, idadi, jinsia, umri na mahali alipowindwa. Kazi hii huhakikiwa
na Afisa Wanyamapori na Mwindaji Bingwa (Profesional Hunter) wa eneo
husika kwa mujibu wa Kanuni za Uwindaji wa Kitalii.
c) Tuhuma kuhusu idadi ya wanyama walioruhusiwa kuwindwa ikiwemo kuuwa tembo wanane (8)
Pamoja na familia ya Freidkin
kupewa leseni ya Rais kuwindia, hakuna tembo yeyote wala Simba
aliyewindwa. Tuhuma kwa Familia ya Freidkin kuwinda Tembo wanane na
simba si za Kweli. Tuhuma hizo zilikuwa na nia ovu ya kumchafua,
kumdhalilisha Mheshimiwa Waziri Nyalandu pamoja na familia ya Freidkin.
Ukweli ni kwamba pamoja na kuwa
idadi ya wanyama hao walikuwa wameandikwa kwenye leseni iliyotolewa,
lakini wanyama hao hawakuwindwa kwa sababu hawakuwa wamefikia ubora wa
Nyara inayotakiwa kuwindwa kisheria.
Kwa mujibu wa Sheria na Kanuni za uwindaji nchini, mnyama tembo
anaruhusiwa kuwindwa kwa ajili ya matumizi binafsi na siyo ya
kibiashara. Kufuatana na Mkataba wa CITES, Tanzania imekuwa ikiwinda
tembo 50 kwa miaka ya 1990 na baadaye kwenye miaka 2000 tembo 200 idadi
ya tembo ilipoongezeka.
Hata hivyo, mwezi Juni 2014 Mhe.
Waziri wa Maliasili na Utalii alipunguza idadi hiyo kwa asilimia 50%
kutokana na kupungua kwa idadi ya tembo wenye ubora wa kuwindwa. Aidha,
uwindaji huo unazingatia viwango vilivyowekwa kwa mujibu wa Kanuni za
Uwindaji wa Kitalii. Endapo tembo aliyeandikwa kwenye kibali au leseni
hajafikisha viwango stahiki hatawindwa.
d) Tuhuma ya Kuruhusu wageni kuwinda katika vitalu ambavyo siyo vya kampuni husika
Tuhuma hizi si za kweli.
Tuhuma hizi zina nia ovu ya kudhoofisha kasi ya kupambana na ujangili.
Ukweli nu kuwa, Freidkin na
familia yake waliruhusiwa kuwinda kwenye vitalu vya Lake Natron, Makao
open na Makao Wildlife Management Area (WMA), Maswa Kimali na Maswa
Mbono kwa sababu hii ndiyo maana Freidkin na familia yake walipewa
Leseni Maalum/Leseni ya Rais kwa mujibu wa Tangazo la Serikali Na. 243
la mwaka 2010 Kanuni ya 19(2) ambalo linaeleza kuwa mwenye Leseni ya
Rais anaruhusiwa kuwinda eneo lolote kama atakavyoelekeza Mkurugenzi wa
Wanyamapori. Kwa mantiki hii, si kweli kwamba Mheshimiwa Waziri Nyalandu
alikiuka sheria na kugawa zaidi ya vitalu vitano vya kuwindia kwa
familia ya Freidkin.
Hivyo, tuhuma ya kuwa Waziri
Nyalandu amekiuka kifungu kinachoweka ukomo wa idadi ya vitalu ambavyo
ni vitalu vitano kwa kampuni si za kweli.
Kwa kuzingatia maelezo hayo hapo
juu, kutolewa kwa leseni ya Rais kwa familia ya Freidkin kulizingatia
sheria, kanuni na taratibu zote za uwindaji.
Tuhuma zote zilizotolewa dhidi ya
Wizara ya Maliasili na Utalii na Mheshimiwa Waziri Nyalandu kuhusu
utoaji wa Leseni ya Rais ya kuwindia kwa familia ya Freidkin, zilikuwa
na nia ovu ya kuchafua, kudhalilisha na kushusha heshima ya Wizara ya
Maliasili na Utalii, na Mheshimiwa Waziri Nyalandu na familia ya
Freidkin
e) Tuhuma kuwa Waziri Nyalandu
ameruhusu Tanzania Game Trackers Safari (TGTS) kumilikishwa vitalu
vinane pamoja na eneo la wazi na hivyo kukiuka kifungu cha 38(7) cha
sheria ya wanyamapori Na. 5 ya mwaka 2009 pia si za kweli.
Ukweli ni kuwa kampuni ya Tanzania
Game Trackers Safari (TGTS) ndiyo iliyotumika kuwindisha familia ya
Freidkin kwenye maeneo matano yaliyotajwa juu na si vitalu vinane kama
ilivyoandikwa na gazeti la Jamhuri.
Vilevile kama ilivyoelezwa hapo juu kisheria, mtu mwenye leseni
ya Rais ya uwindaji anaruhusiwa kuwinda eneo lolote linalofaa kuwinda
kisheria bila kujali ukomo wa idadi ya vitalu.
Tuhuma hizi zilikuwa na nia ovu ya kuchafua, kudhalilisha na
kushusha heshima ya Wizara ya Maliasili na Utalii, na Mheshimiwa Waziri
Nyalandu na familia ya Freidkin
f) Tuhuma ya kuwa Waziri
Nyalandu ameruhusu uwindaji wa kitalii kufanyika eneo la Makao, sehemu
ambayo haijatengwa kama kitalu pia si za kweli.
Tuhuma hizi zinalenga kuchafua jina zuri la Mheshimiwa Waziri na kumpunguzia dhamira, Hari na kasi ya kupambana na ujangili.
Ukweli ni kuwa, eneo la Makao
pamoja na kwamba halijatengwa rasmi kama kitalu cha uwindaji, lakini
kisheria linaruhusiwa kufanyika shughuli za uwindaji (yaani kwa lugha
iliyozoeleka – kuwindwa) kama ilivyo kwa maeneo mengine ya mapori
tengefu na mapori ya wazi. Hii ndiyo maana familia ya Freidkin
haikugawiwa vitalu bali ilipewa kibali cha kuwinda katika maeneo
yaliyotajwa.
2. Katika gazeti Jamhuri la
tarehe 30 machi 2014 toleo namba 129 ilichapishwa taarifa potofu yenye
kichwa cha habari NYALANDU ’ AUZA’ HIFADHI
· Yeye na lembeli waenda afrika kusini kukamilisha mpango
· Katibu mkuu njia panda alazimishwa kuidhinisha safari, posho
· Hifadhi nyingine nazo mbioni kutolewa kwa wawekezaji
Taarifa hiyo potofu ilielezea kuwa Waziri Nyalandu alikwenda
nchini Afrika ya Kusini na kufanya mazungumzo na kampuni ya African
Parks Network (APN) kwa ajili ya kuikabidhi uendeshaji wa Hifadhi za
Taifa, Mapori ya Akiba na Mapori Tengefu ikiwemo kuuza hifadhi ya
Katavi.
Tuhuma hizi si za kweli.
Tuhuma hizi zililenga kuchafua
jina la Wizara ya Maliasili na Utalii na kumchafua mheshimiwa Lazaro
Nyalandu, Waziri wa Maliasili na Utalii.
Ukweli ni kuwa Safari ya Waziri
Nyalandu kwenda Africa kusini ilikuwa rasmi na ilifuatia maagizo ya
Serikali kuhudhuria mkutano wa African Parks Network (APN) wa uhifadhi
ulioandaliwa na asasi hiyo kwa lengo pia la kuhakiki uwepo, utendaji
halisi wa taasisi hiyo na kufanya majadiliano kuhusiana na mapendekezo
yao.
Huu ni utaratibu wa kawaida wa utendaji serikalini ambapo taarifa ya safari hiyo iliwasilishwa Serikalini kwa hatua zaidi.
Katika mkutano huo, hakukuwa na
mikataba yoyote iliyowekwa na Waziri Nyalandu au maamuzi yoyote ya
kukabidhi hifadhi za Taifa kama ilivyoelezwa na gazeti la Jamhuri.
Tuhuma hizo zilizolenga kuchafua jina la Wizara ya Maliasili na Utalii na Mhe. Nyalandu.
3 Gazeti la Dira jumatatu,
Machi 31 – April 6, 2014, liliandika habari yenye kichwa cha habari
“Kashfa za Nyalandu zatikisa. Na vichwa vidogo vya habari vilivyosomeka,
Adaiwa kumiliki vitalu, kampuni ya “tours”, Aificha chini ya mwamvuli
wa Wachina.
Tuhuma hizi si za kweli.
Tuhuma hizo zina nia ovu ya kuchafua jina la Mheshimiwa Waziri Nyalandu na kupunguza kasi yake ya kupambana na ujangili.
4 Taarifa ya kuwa Waziri
Nyalandu anatuhumiwa kurefusha msimu wa muda wa uwindaji kuanzia Julai
Mosi hadi Machi 30 ambapo ni sawa na muda wa miezi tisa kila mwaka
tofauti na muda wa kisheria ambao ni kuanzia Julai Mosi hadi Decemba 31
sawa na miezi 6 kwa mwaka si za kweli.
Ukweli ni kwamba Waziri Nyalandu alitangaza kusudio la kuongeza
msimu wa uwindaji kutoka miezi sita kwenda tisa na hii iko ndani ya
mamlaka ya waziri kisheria kama ilivyo kwenye Sheria ya wanyamapori
namba 5 ya mwaka 2009 na kanuni zake.
Hii siyo mara ya kwanza kwa mawaziri wenye dhamana ya Maliasili na Utalii kurefusha au kufupisha msimu wa uwindaji.
5 Tuhuma ya kuwa Waziri
Nyalandu ni mmoja wa wafanyabiashara wa Uwindaji na yuko karibu kabisa
na wawindaji wenye vitalu nchini hazina ukweli wowote.
Waziri Nyalandu ni waziri mwenye
dhamana ya kusimamia masuala yote ya Maliasili na Utalii na anapaswa
kuwa karibu na wadau wote wa maliasili na Utalii ili kuweza kusimamia
vema sekta hiyo. Huwezi kuisimamia vema Sekta husika kwa kuwakwepa wadau
husika.
6 Tuhuma ya kuwa Waziri Nyalandu anakabiliwa na kashfa ya kujihusisha na ujangili mkoani Singida pia si za kweli
Ukweli ni kuwa tuhuma hizo
zina nia ovu ya kuchafua jina la Waziri Nzyalandu, kumshushia heshima na
hadhi yake kwa lengo la kupunguza na kukwamisha jitihada zake za
kukabiliana na ujangili uliokithiri hususan mauaji ya tembo na faru.
Jitihada zilizofanywa na
Waziri Nyalandu hadi sasa ni pamoja na kutafuta fedha na vifaa ndani na
nje ya nchi ikiwemo helikopta moja na kuwezesha kuanzishwa kwa mfuko
maalum wa kukusanya fedha kutoka kwa wadau wa maendeleo chini ya uratibu
wa shirikal a Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) ofisi ya Tanzania.
7 Kashfa za kumhusisha Waziri
Nyalandu na Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Mwanyonye, Rehema Manji kudai
kuwa alitishiwa bastola ni kosa kisheria kwani. Waziri Nyalandu hakuwahi
kutenda kosa hilo.
Kutajwa kwa mmiliki wa gari namba T
505 BKM kuwa ni la ndugu Lazaro Samwel Nyalandu, mwenye utambulisho wa
mlipa kodi (Tin: 105-059-701) si uthibitisho ya kuwa Waziri Nyalandu
alihusika kumtishia bastola Rehema Manji. Kashfa hizo zililenga
kumchafua, kumshushiaa hadhi Waziri Nyalandu.
8 Katika gazeti la Jamhuri la Jumanne October 07 – 13, 2014
ISSN No. 1821-8156 Toleo No. 157, zilichapishwa taarifa zenye kichwa cha
habari AUNTIE EZEKIEL ATANUA NA NYALANDU MAREKANI.
Tuhuma hizi si za kweli. Tuhuma
hizi zimetolewa na watu wenye nia ovu na zimelenga kuchafua jina la
Wizara ya Maliasili na Utalii na kumchafua mheshimiwa Waziri Lazaro
Nyalandu, kumshushia Heshima, kumdhalilisha kwa umma ili kumpunguzia
dhamira, malengo na kasi ya kupambana na ujangili.
Ukweli ni kuwa, Waziri Nyalandu
hakuhusika kwa namna yoyote ile na kile kilichoelezwa na gazeti la
Jamhuri “Aunty Ezekiel atanua na Nyalandu Marekani” kichwa cha habari
hiyo na vichwa vidogo vya habari vilivyoandikwa vililenga kutoa picha
potofu kwa umma ili kumchafua, kumdhalilisha, na kuvuruga amani kwa
Waziri Nyalandu na familia yake.
Waziri wa Maliasili na Utalii,
akiwa nchini Marekani kikazi, alialikwa kuhudhuria shughuli ya kutimiza
miaka minne ya blog ya Vijimambo ambayo inamilikiwa na Watanzania
waishio Marekani.
Waandaaji wa shughuli hiyo
iliyolenga kutangaza Utalii wa Tanzania nchini Marekani walimwalika
Waziri Nyalandu kuwa mgeni rasmi. Mwaka jana kwenye sherehe kama hizo
alialikwa Rais mstafu Ali Hassan Mwinyi
Wizara ya Maliasili na Utalii haikuhusika na uratibu wa safari ya Msanii Auntie Ezekiel.
Tarifa hizo zimelenga kuchafua Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na Mheshimiwa Waziri Lazaro Nyalandu.
Tuhuma za ufisadi, ujangili na
matumizi mabaya ya madaraka hazina ukweli wowote. Tuhuma hizo zinalenga
kudhoofisha kasi ya Waziri Nyalandu katika kupambana na ujangili.
9 Hoja ya kuwa waandishi wa
habari wameshinda na kuwa wameokoa mamilioni ya fedha za umma ambazo
zingetumika kulipia mkutano na badala yake mkutano huo ulifanyikia
wizarani hazina msingi.
Hoja hizo si za kweli kwa kuwa Mheshimiwa Waziri Nyalandu anatumia kumbi za wizara kufanya mikutano na wadau.
Mikutano ya wizara ya Maliasili na
Utalii inayofanyikia kwenye kumbi za mikutano nje ya wizara, inafuata
taratibu zote za Serikali na inategemeana na idadi ya washiriki wa
mikutano hiyo na aina ya mkutano husika.
Utaratibu huu ni wa kawaida na
hutumiwa na watendaji na viongozi mbalimbali wa Serikali na si upotevu
wa fedha za umma kama inavyodaiwa na magazeti husika bila kujua uhalisia
wa mikutano, idadi ya watu watakaohudhuria mkutano , na wadau wa
mkutano husika.
Mikutano hii imekuwa na manufaa makubwa kwa taifa katika swala zima la kupambana na ujangili
10 Tuhuma ya kuwa waziri
anafanyia kazi hotelini si za kweli kwa sababu kiongozi wa serikali wa
ngazi za juu anakuwa kazini muda wote bila kujali yuko wizarani ama nje
ya wizara.
Tuhuma hizo zinalenga kuchafua
jina zuri la Waziri Nyalandu, kumkatisha tamaa na kumpunguzia heshima
yake kwa umma ili kupunguza kasi yake ya kupambana na ujangili.
Hadi sasa kuna mafanikio makubwa
yaliyojitokeza katika suala zima la kupambana na ujangili ikiwemo
Kupungua kwa kiasi kikubwa kwa mauaji ya tembo. Idadi ya tembo katika
ikolojia ya Serengeti – Maasai Mara imeongezeka, kupungua kwa matukio ya
ujangili katika Pori la Akiba Selous kuanzia mwezi machi 2014 hadi
sasa, wadau wengi kujitokeza katika kusaidia suala zima la kupambana na
ujangili wa wanyamapori nchi kama Marekani, Ujerumani, China, Uingereza.
Wizara ya Maliasili na Utalii
inatoa taarifa kwa umma kwamba tuhuma zote zilizotolewa na hata
zitakazoendelea kutolewa na gazeti la Jamhuri dhidi ya Wizara ya
Maliasili na Utalii na dhidi ya Waziri wa Maliasili na Utalii Mheshimiwa
Lazaro Nyalandu zinalenga kulichafua jina la Wizara ya Maliasili na
Utalii na pia kuchafua jina la Mheshimiwa Waziri Lazaro Nyalandu na
hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya gazeti la Jamhuri na
chombo chochote cha habari kitakachotoa taarifa za kuchafua jina la
Wizara ya Maliasili na Utalii na Waziri wa Maliasili na Utalii
Mheshimiwa Lazaro Nyalandu.
0 comments:
Post a Comment